A lady using sign language infront of a laptop

Kuhusisha Watu Walio na Ulemavu Kwenye Mtandao

KICTANet, shirika la kijamii, limekuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha ushiriki wa watu wenye ulemavu kwenye mitandao. Mwamko huu umetokana na malengo ya shirika hili, ambayo ni pamoja na kuangazia sera za mawasiliano na mifumo ya kidijitali, utetezi wa haki, uelimishaji na uwezeshaji, na ushirikiano na wadau wengine kwenye mtandao

Kupitia mpango wake wa Digital Accessibility, KICTANet imehusisha watu wenye ulemavu katika uongozi wa mtandao nchini. Hii imewezesha watu wenye ulemavu kuchangia katika njia za kutumia mifumo ya kidijitali na kueneza wito wa kujumuishwa kwenye masuala ya mitandao.

Mtandao unapaswa kuwa wazi kwa matumizi ya kila mtu bila ubaguzi. Mtandao una uwezo wa kufikia kila mtu iwapo sera na sheria zinazingatiwa, na pia una nguvu za kuwawezesha wananchi kujiendeleza kiuchumi na kielimu.

Changamoto kwa Walio na Ulemavu

Hata hivyo, bado kuna changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu. Licha ya nia yao kubwa ya kutumia mitandao, uwezo wao unakabiliwa na changamoto kama vile ukosefu wa vifaa vya usaidizi (kwa Kiingereza Assistive devices), ukosefu wa elimu, na gharama ya kuunganishwa kwenye mitandao.

Hii imechangia watu wenye ulemavu kukosa fursa muhimu mtandaoni, kama vile biashara, elimu, huduma za serikali, na burudani. Pia inaathiri maisha yao hasa kwa wale wanaotegemea mtandao kwa shughuli za msingi, kama vile kuwasiliana na kusafiri.

Kwa kina, ukosefu wa uwezo wa kutumia mtandao umekuwa changamoto kubwa. Kwanza ni kukosa ujuzi na mafunzo ya jinsi ya kutumia mtandao na vifaa vya kidijitali. Pili ni gharama ya vifaa na ya kujiunga na mtandao. Ingawa gharama ya mtandao inaweza kuonekana kuwa sawa kwa kila mwananchi, ni muhimu kukumbuka kuwa watu wenye ulemavu pia wana mahitaji mengine zaidi ya mahitaji ya msingi, kama vile magurudumu na fimbo za kutembea, vipulikizi kwa wasiosikia, mafuta ya kulinda ngozi dhidi ya miale ya jua kwa walio na ulemavu wa ngozi, miwani, breli n.k.

Kwenye ripoti yao ya Accessibility of Government Websites to Persons with Disabilities, KICTANet imebainisha kuwa mtandao, hususan tovuti, una ugumu wa matumizi (inaccessibility kwa Kiingereza). Hii inatokana na jinsi tovuti hizi zilivyoundwa bila kuzingatia mahitaji na upungufu wa walemavu, kama vile kutokuona, kutosikia, na kukosa viungo kama mikono. Hali hii inawanyima walemavu fursa za kujihusisha na huduma muhimu za serikali na kuendeleza maendeleo yao mtandaoni.

Kwa kuongezea, kuna upungufu mkubwa wa sera na sheria zinazoelekeza kujumuisha walemavu katika masuala ya kidijitali. Hata zile chache zilizopo hazitekelezwi kikamilifu, na wengi wanazipuuza.

Ni Njia zipi Bora za Kuakisha Walemavu Wanashiriki Kikamilivu kwenye Mtandao?

Kwanza, ni wito wa kuwahusisha na kushirikiana na watu walio na ulemavu katika masuala ya uongozi, ubunifu, na matumizi ya mtandao. Wanajua changamoto zinazowakabili vyema, na wanafahamu mahitaji yao zaidi.

Pili, ni ombi kwa wadau wote kuendelea kusambaza ujumbe na kuelimisha umma na jamii kuhusu umuhimu wa kuhusisha na kushirikisha watu walio na ulemavu kwenye mtandao. Waeneze sauti kuwa walemavu wana haki, uwezo, na uzoefu wa kutumia mtandao.

Tatu, tunahitaji kuweka programu za mafunzo na maelekezo kwa watu walio na ulemavu ili waweze kujifunza jinsi ya kutumia mtandao na teknolojia zinazohusiana. Hii itasaidia kupunguza kutengwa kwao kupitia elimu na kuwapa uwezo wa kushiriki kikamilifu kwenye mtandao na vifaa vya kidijitali

Hatimaye, kwa sisi wenye ulemavu, ni wakati wa kujitokeza, kuongea kwa sauti moja, kuwakilisha masilahi yetu kwa ufasaha, na kusimama imara kutetea haki zetu za kidijitali. Tuna jukumu la kuwa mstari wa mbele kufanya mabadiliko na kusimamia maslahi yetu kwenye ulimwengu wa kidijitali.

Nicodemus Nyakundi ni Mshirika wa Upatikanaji na Usawa wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) kwa Watu Wenye Ulemavu (PWDs) katika KICTANet. Ana historia ya taaluma katika Teknolojia ya Habari (IT) na anatetea ushirikishwaji wa kidigitali.

Loading

Nicodemus Nyakundi information

Digital Accessibility Program Officer at KICTANet. He has a background in Information Technology, and is passionate about digital inclusivity.

Related Posts

Submit a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.